top of page

Hillary na Trump

Hillary Clinton ameteuliwa rasmi na chama cha Demokrat kupigania kiti cha urais wa Amerika. Vilevile wanaRepublikan wamemchagua Donald Trump kuwa mgombea wao. Uchaguzi mkuu ni tarehe 8 Novemba, 2016. Mmoja wa hawa wawili atakuwa rais na hiyo itakuwa historia.

Hillary Clinton atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini Amerika. Mwanamke wa kwanza katika miaka 240 ya uhuru wa nchi. Ndiyo, Liberia, Brazil, Malawi, Ujerumani, India, na nchi nyingine nyingi zimepata kumchagua mwanamke ila Marekani. Donald Trump akichaguliwa atakuwa mgombea urais ambaye hajashikilia kiti chochote cha kisiasa. Trump ni bepari anayefanya biashara ya ujenzi.

Nimefuatilia harakati za uteuzi rasmi wa vyama hivi viwili kupitia kituo cha televisheni cha Cable-Satellite Public Affairs Network (CSPAN). Nimezisikiliza hotuba karibu zote na nimefuatilia shughuli zote za uteuzi. Asante CSPAN kwa mfululizo wa matangazo bila matangazo ya biashara au kelele ya wachanganuzi wa kisiasa.

Mikakati ya vyama hivi viwili imekuwa kama usiku na mchana mwaka huu. Republikan walipokutana mjini Cleveland walilalamika nchi ina udhaifu na imezorota sana chini ya Rais Baraka Obama. Walidai nguvu ya himaya ya Amerika inahatarishwa na Urusi, Uchina, magaidi, na watu wanaohamia Amerika kutoka nchi zingine. Walisema Hillary ni mwongo na mhalifu. Vigogo wengi wa chama hicho walisusia kongamano kupinga uteuzi wa Trump. Wanamuona kama mtu asiyewasilisha maadili yao.

Viongozi wa Demokrat wakikutana mjini Philadelphia wana matumaini makubwa kuwa nchi ya Amerika inaendelea kuwa yenye nguvu kutokana na kuwakubali na kuwaheshimu watu wenye tofauti za kidini, kiasili, kijinsia, kimapato, n.k. Rais Obama alikiri Hillary ndiye mgombea kiti anayefaa na mwenye tajriba bora kuliko mgombea yeyote katika historia ya nchi. Aliyekuwa Meya wa jiji la New York, Michael Bloomberg, hata alidai Donald Trump ni tapeli na huenda akawa hana akili timamu. Lo! Makali hayo! Lakini matamshi yake yanaelekea yeyote kushuku utimamu wake kiakili. Vigogo wote wa chama hiki walifika kumuunga mkono Hillary na kutetea maadili ya wdemokrat: kuwatetea wanyonge.

Inaonekana wengi wanaomuunga mkono Trump ni wazungu wanaogopa kuwa watu wa mataifa na asili tofauti wanaendelea kubadilisha taifa. Haki za walemavu, weusi, wanawake, wahamiaji, waislamu na wengineo zinabadilisha nguvu za wanaume wazungu ambao wamependelewa na hali ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa tangu zama za zamani. Wanaogopa mabadiliko yanayoendelea kuifanya Amerika nchi yenye kuwapa hadhi wengi sio wachache.

Kongamano zimekwisha. Wagombea urais na makamu wao wameteuliwa: Tim Kane na Hillary, Mike Spence na Donald Trump. Sasa kinyang'anyiro kinaanza kwa fujo. Uchaguzi huu utakuwa mchafu. Uamuzi wa wapiga kura utaamua iwapo Amerika itakuwa nchi ya amani ama ya vitisho. Nchi yenye utangamano wa watu tofauti ama yenye uhasama dhidi ya walio tofauti.

Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page