top of page

Hillary Clinton na Trump: Raundi ya Pili katika Wash U


Haya karibuni kwetu Wash U (Washington University in St. Louis) kwa raundi ya pili ya mchuano wa kisiasa baina ya Hillary na dubwana Trump. Kwenye televisheni ama ukumbuni Wash U karibuni kumsikiliza Hillary na dubwasha wakizungumza kuhusu mambo watakayoyafanya wakishinda uchaguzi wa urais. Bila shaka wengi tunampendelea Hillary kwa sababu zilizo wazi. Jamaa yule wa mahanjam na matusi anaweza kutuletea matatizo mengi duniani akishinda. Amekwisha sema ukweli wake na wafuasi wake watataka atimize yale aliyoahidi. Tusidanganywe eti atabadilika akichaguliwa. Wanaosema hivyo na wale watu watakaokuuzia kondoo na kukuahidi kuwa atageuka kuwa farasi akifika kwako. Kumbuka ndio wale wale walisema Trump akiteuliwa kuwa mgombea kiti cha urais atabadilika. Ukweli tumeuona.

Sasa hapa kwetu Wash U tumekuwa tukijiandaa kwa wiki kadha. Kuandaa pia ni ngoma yenye kasheshe zake. Mkono wa serikali umejidhihirisha kuhakikisha kwamba usalama umeimarika. Wamekuweko polisi na makachero kochokocho. Baadhi ya majumba, hasa yaliyo karibu na jumba la mdahalo, yamezingirwa kwa ua (fence) la chuma. Kuingia chuoni lazima tuonyeshe kitambulisho cha chuo.

Lakini palamiki. Tumeyazoea. Wash U iliandaa mdahalo wa George Bush na Al Gore (wamkumbuka?), George Bush na John Kerry, na Joe Biden na Sarah Palin (yule mama anayeona Urusi kutoka Alaska). Ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wetu kujifunza kuhusu maswala ya kisiasa na pia kuona wanahabari wakiyapeperusha matangazo yao moja kwa moja. Sisi walimu hatupewi tiketi za kuingia ili wanafunzi wengi wawezekuhudhuria. Na inafaa kuwa hivyo.

Biashara mjini St.Louis pia hunufaika si haba. Wageni wengi watafika na kulala mahotelini. Kutoka wanahabari, maofisa wa serikali, wanaharakati, vigogo wa vyama,na wengineo watafika. Mikahawa na vilabu vitahesabu mapeni zaidi. Na sijataja vile chuo chetu kitafaidika kwa kupata sifa.

Ukifika Wash U kwa mdahalo, usisahau kutusalimia. Na lazima watu wenye kura wajitokeze na kupiga kura siku ikifika. Mimi niko naye Hillary. Na siogopi kusema hivyo.

Dkt. Mungai Mutonya anafundisha Washington University in St.Louis na ni mwandishi wa vitabu vya Kiswahili. Pia anachapisha blogu ya Kiswahili <http://mmutonya.wixsite.com/blogu>

Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page