top of page

Msako kwenye Daraja la Mississippi


Chain of Rocks Bridge

Ujumbe waWhatsApp ulikuwa mfupi: "Zawadi hajapatikana bado. Tukutane kesho asubuhi kwenye OCOR kusaidia msako. Asanteni."

Siku iliyofuata manyunyu ya mvua na upepo uliotamani kutupokonya miavuli yetu hazikutuzuia kuendelea na msako wetu. Tulikuwa katikati ya daraja linalowawezesha watembeaji miguu kuvuka mto Mississippi ambao ni mpaka wa majimbo ya Illinois na Missouri. Habari za televisheni na magazeti zilisema kando ya daraja ndipo Zawadi aliliacha gari lake.

Polisi walikuwa wametumia mbinu tofauti za usakaji bila mafanikio. Siku ya tatu jamii ya Wakenya mjini St. Louis ilijitokeza kumtafuta Zawadi. Msichana aliyejulikana kwa tabasamu lake lililoyeyusha shaka, werevu uliomwezesha kujiunga na chuo kikuu mashuhuri hapa mjini, na heshima iliyowapendeza waliomjua. Lakini sasa katoweka na hakuna anayejua ameenda wapi. Simu yake ilienda mteja kila mara.

Inawezekana alitoroka tu nyumbani? Inawezekana alitekwa nyara? Ama ametoroka kuolewa? Anaweza kuwa amejificha kwa siku tatu kwenye vichaka vilivyo chini ya daraja hili kubwa? Ama alivuka upande wa pili wa daraja na kuendelea na safari ya alikotaka kwenda? Inawezekana aliruka futi hizo zote kutoka darajani hadi kwenye mto huu mkubwa sana? Maswali yalitusonga na hakuna aliyekuwa na jibu. Ama kuna wale waliokuwa na habari za undani zaidi lakini walisita kueleza kinagaubaga. Msako wetu ukaendelea.

Manyunyu yakatutonesha. Kando ya mto tukasaka. Chini ya magongo ya miti tukachunguza. Vichakani pia tukachungulia na kuita. Miguu yetu ikakwama matopeni. Tukajikwamua na kuendelea. Hatimaye, mvua ikazidi na matope yakawa kikwazo kukubwa.

Msimu wa mvua wa mwezi wa Aprili uliendelea na mto Mississippi ukafurika. Polisi waliendelea na msako wao. Jamii iliendelea na maombi na harambee ya kuwafariji wazazi waliokuwa wakikabiliana na kumbo lisiloelezeka.

Hatimaye, ripoti ilifika. Ripoti ya polisi ambayo iliikata matumaini ya wote waliotamani kumwona Zawadi tena akiwa hai. Misa ya wafu na harambee zilifanyika siku ya Jumamosi tarehe 21. Wazazi wataenda kumlaza Zawadi nyumbani Kenya. Mto Mississippi ulimmeza Zawadi lakini baadaye ulimkabidhi kwa polisi, wazazi wake, na jumuiya iliyojawa na majonzi.

Kilichotokea kwenye daraja la Mississippi siku alipotoweka Zawadi hatujui. Ila tunalolijua ni kuwa jamii ya wakenya mjini St. Louis imeshangazwa na kuhuzunika kumpoteza msichana mwenye haiba na matumaini makubwa. Mola ilaze pema peponi roho yake Zawadi. Mola azidi kuwapa nguvu wazazi na familia yote nguvu za kukabiliana na janga hili.

Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page