top of page

Mapenzi ya Facebook-1


Jason aliufungua ukurasa wake wa Facebook kwa mara ya sijui-ngapi siku ya leo. Kila mara alipofungua moyo ulimdunda na akahema kwa matarajio. Kila wakati alifikiri angepata majibu ya ujumbe alioutuma baada ya ombi lake la urafiki kukubaliwa. "Niwie radhi kwa kuuliza" aliandika kwa unyenyekevu na wasiwasi "wewe ndiye Halina Wasiku kutoka Thika? Halina aliyesomea Gatimu, Alliance, na UoN?" Aliongeza swali la mwisho kusudi isiwe kuna Halina Wasiku mwingine kutoka Thika. Alitaka kumwambia mengine mengi lakini alitaka kuwa na hakika Halina huyu aliyempata mtandaoni alikuwa kweli ni Halina aliyemjua miaka kumi iliyopita. Halina aliyeuteka moyo wake kwa tabasamu za kuyeyusha, kwa macho yake ya gololi, kwa urembo wake wa malaika, na kwa kicheko cha kusisimua. Sasa imetimu miaka kumi bila kumwona wala kuwasiliana naye. Pengine tafutatafuta zake zilizokuwa zimeambuliwa patupu huenda zikafua dafu.

Kwa kawaida Jason hapendi kuandika mengi kwenye ukurasa wake. Facebook kwa maoni yake ni jukwaa la kupata habari na udaku kuhusu ndugu na marafiki ambao wanapenda kuanika maisha. Hafahamu ni kwa nini binamu hachoki kutundika picha tofauti za uso wako kila mara kwenye Facebook. Pengine ila apate kujua wangapi wataipenda picha. Hafahamu ni kwa nini rafiki yake anapenda kutundika picha za watoto wake wadogo wakifanya hili au lile. Hajui kuna mazimwi mtandaoni? Lakini hajali kuona yote kwa vile anapata habari zao bila hata kuuliza. Anajua rafiki yake Karis alitembelea mji wa Kampala, alihudhuria arusi ya aliyekuwa mpenzi wake, alijaribu kupigania kiti cha ubunge lakini hakupata hata tikiti ya chama kwenye mchujo. Dadake mdogo naye alikuwa Three Rivers Mall na akanunua rinda na kula kuku na chipsi. Habari zote kutoka mapitio ya kurasa za Facebook.

Lakini juzi alikuwa anafululiza kuzisoma kurasa na wenye ndipo akaona binamu yake, Carol, ameipenda picha ya Halina Kibwana. Roho ikamruka kidogo. Carol na Halina Wasiku walisoma shule ya sekondari pamoja. Hata alikuwa anamtuma Carol kumfikishia jumbe Halina. Je, yawezekana Halina Kibwana ni Halina Wasiku? Ameolewa? Yuko wapi siku hizi? Alijua Carol na familia yake wanaishi mjini Mombasa. hwajawalisiliana kwa muda pia.

Akaufungua ukurasa wa Facebook wa Halina Kibwana. Akaupitia huku moyo unamdunda akitaka kujua kama ni Wasiku. Picha zilizokuwemo ni nukuu zilizorembeshwa na mandhari ya kuvutia - milima, bustani, fuo za bahari, nyumba maridadi, na kadhalika. Hakukuwemo picha za kibinafsi. Akajaribu kufungua sehemu ya picha lakini hakuweza kwa vile hawakuwa marafiki wa Facebook. Akajaribu kuutuma ujumbe lakini hali ikawa vilevile. Akaona hana lingine ila kutuma ujumbe wa kuomba urafiki. Akabonyeza.

Itaendelea kwenye sehemu ijayo.

Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page