top of page

Trayvon Martin Mtaani Zimmerman, Nairobi


Black Lives Matter Demonstration

Mahakama imeamua George Zimmerman hana hatia. Maandamano yatanda kote nchini kupinga uamuzi huo. Ghasia zazuka na waandamanaji waharibu mali. Mamilioni watia sahihi ombi la kumtaka Mkuu wa Sheria, Eric Holder, amfungulie Zimmerman mashtaka mapya. Kwenye vipindi vya televisheni watu warushiana maneno makali na kukashifiana. Kwenye kurasa za Facebook na Twitter weusi na weupe wapakana matope na kutukanana vibaya. Hamkani si shwari tena hapa Ughaibuni. Cheche za moto wa ubaguzi wa rangi zalipuka.

Nikawaza. Je, kijana Trayvon Martin angalitembelea mtaa wa Zimmerman ama mitaa ya wenyenazo jijini Nairobi, angalishukiwa kuwa jambazi na kuuawa? Bila shaka hatuwezi kulijibu swali hilo ipasavyo. Wengine watasema kalamu ya Mungu haikosi. Wengine watasema hangaliweza kutembelea Nairobi kwa vile angaliona onyo la Wizara ya Maombi ya Nje na Ubalozi wa Marekani nchini Kenya. Onyo hilo ambalo limekuwepo tangu mwaka 2003 linawaonya Wamarekani wasizuru sehemu tajwa za Kenya. Kwa maoni ya maafisa wa kiserikali kuna hatari ya ugaidi, utekaji nyara, na hatari zinginezo Nairobi na sehemu zisizo za kitalii. Lakini hebu tufikiri Trayvon angelipuuza onyo hilo, kama wafanyavyo Wamarekani wengi, na kuzuru mitaa ya kifahari jijini Nairobi.

Kwanza hebu turejelee uhasama na matusi baina ya Weusi na Weupe tuliotaja hapo juu. Mamangu angaliniadhibu vikali kujua kuwa nayasoma maneno machafu hivyo. Angenilazimisha nimwone padre na kuzitubu dhambi hizo. Lakini siusomi uchafu wa matusi hayo kwa kuwa mimi ni mkaidi na mtovu wa maadili. La hasha! Miye mtu mzima, msomi, mhadhiri mwenye heshima zake. Cha muhimu zaidi ni kuwa mimi ni baba mtu. Yaani babake vijana wawili weusi wanaosoma vyuo vikuu hapa Amerika.

Trayvon Martin alikuwa kijana mweusi wa miaka kumi na saba hivi. Aliuawa alipokuwa akielekea nyumbani kwao mwendo wa saa moja usiku hivi. Aliyemuua, George Zimmerman, ameachilia na mahakama na kuarifiwa kuwa hakuwa na hatia yo yote. HANA HATIA YO YOTE!? Kamuua binadamu! Trayvon alikufa! Trayvon si mnyama!

Trayvon alikuwa ameenda dukani kumnunulia nduguye lawalawa na soda. Alikuwa anarudi nyumbani mwendo wa saa moja jioni kuwahi mchezo wa mpira wa kikapu kwenye runinga. Zimmerman alimwona na kumshuku kuwa jambazi. Eti kwa vile alikuwa kijana mweusi! Akamwandama na hatimaye kumlenga risasi moja ya kifua. Kuachiliwa huru kwa aliyemuua kijana mweusi asiyekuwa na hati kumeibua hisia mbichi za ubaguzi wa kisheria dhidi ya vijana na wanaume weusi nchini Amerika.

Wenye kuunga mkono kuachiliwa huru kwake Zimmerman, wengi wao wakiwa wazungu, wanadai alihofia maisha yake alipompiga Trayvon risasi. Wenye kumtetea Trayvon, asilimia kubwa ikiwa ni weusi, wanakumbushwa visa kochokocho vya ubaguzi wa rangi vinavyoendelea na kuhalalishwa na sheria humu Marekani.

Asilimia kubwa ya wafungwa nchini Marekani ni Weusi. Wengi wakiwa wamefungwa kwa makosa madogomadogo. Polisi wengi wanawasimamisha madereva weusi bila sababu yo yote. Ni kana kwamba ni hatia kuwa mweusi, kuendesha gari, ama kutembelea sehemu wanakoishi wazungu wengi.

Hata hivyo, ni muhimu pia kuangazia kuwa weusi wanauwa weusi wenzao kwa kiwango kikubwa katika makazi duni ya mji mikubwa yaitwayo “ghetto”. Jijini Chicago, kwa mfano, watu zaidi ya 200 wameuawa mwaka huu – wengi wao wakiwa ni vijana weusi waliouawa na weusi wenzao. Hali sio tofauti kwenye makazi duni ya weusi katika mjini ya Los Angeles, Washington, D.C., Detroit, Memphis, na kwingineko. Makazi haya ni yale yenye umaskini usiosemekana, uhalifu, ukosefu wa kazi, na madawa ya kulevya. Pengine itafaa serikali za Kiafrika zifuate mfano wa balozi za Marekani na kutahadharisha raia wake wajiepushe na maeneo hayo yenye uhalifu mkubwa.

Kuachiliwa kwake Zimmerman kuliniacha nikiwaza: ni yapi yangalimpata Trayvon Martin endapo angaliitembelea mitaa ya kifahari jijini Nairobi kama vile Runda, Muthaiga, Karen, na Lavington? Je, angalipigwa risasi na polisi wanaopiga doria Karen na kusemekana kuwa jambazi sugu?

Je, askari walinzi wa G4S huko Lavington wangaliyaachilia majibwa yao makali aina ya German Shepherd yamraruerarue kijana Trayvon? Ama kikosi cha Kwekwe kingemwona akitembea mtaa wa Muthaiga na kumshuku kuwa mwanachama wa Mungiki? Kikosi cha Alfa Romeo kingemkamkata abaki kuwa kisa cha kuripotiwa na Mohammed Amin kwenye “Parawanja la Uhalifu”?

Pengine mlinzi angelifungua kidirisha cha lango kuu na kusema “Hei, gichana unagwenda wabi na hii mvua? Wewe iko na botea?” Na pengine angetambua kuwa kijana anaeleka nyumbani kwao na kumwacha aende zake. Ama Mama Njeri angekutana naye akiwa kwenye pilkapilka zake ya kuwauzia walinda usiku chai, mahamri, na virojorojo vingine. Angemwona Trayvon ameloa chepechepe na kusema “Ngai baba, kinjana husikii hiyo mvua. Wooieeee! Si utashikangwo na homa. Kura hii mandathi moja na hii kalatasi ya naironi ufinike hiyo kishwa shako.” Kabla ya kufika nyumbani kwao angepita nyumba ya Mpig inayolindwa na Shirandula. Wangesalimiana kama kawaida na Trayvon angefika nyumbani mapema kuona Harambee Stars ikipimana nguvu na Super Eagles. Mama yake angemkemea kwa kunyeshewa. Babake angekuwa amezama kwenye mchezo, Tusker mkononi, hata hangetambua Trayvon amefika kuchelewa huku ameloa. Trayvon angebadilisha nguo, ajipakulie chajio, na ajiunge na babake kuishangilia Harambee Stars.

Lakini hali haikuwa hivyo kwenye mtaa mmoja wa kifahari katika jimbo Florida. Wala haitakuwa hivyo kwenye mitaa wanapoishi wazungu wengi. Ubaguzi wa rangi ni hatari kubwa sana inayoikabili nchi ya Marekani. Licha ya kuwa nchi inajaribu iwezavyo kuufinika uozo huu wa kijamii, ukweli ni kwamba hali ni mbaya zaidi kuliko hali ya ukabila katika nchi za Kiafrika. Angalau tunakubali tuna shida ya ukabila na tunafanya iwezekanavyo kulikabili tatizo hilo. Huku inakuwa mwiko kuzua mjadala kuhusu ubaguzi wa rangi.

Sheria za Florida na majimbo mengine zinazodai kuwa watu kama Zimmerman hawana hatia, pamoja na uhuru wa raia wa kubeba bunduki, zinatiliwa kiwewe mustakabali wa mahusiano ya watu weusi na weupe hapa Marekani. Ni muhimu kujihadhari!

Tags:

Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page