top of page

Baada ya Cape Town

Baada ya kongamano na safari jijini Cape Town nilirejea nyumbani Kenya. Safari ya kurudi ilibidi kwanza niiruke Kenya hadi Uhabeshi kisha nifululize hadi Nairobi. Lakini sikujali kwani niliiona kuwa fursa ya kufika jiji la Addis Ababa, jiji lenye makaa makuu ya Umoja wa Nchi za Kiafrika (AU). Nilipata fursa ya kufika hoteli moja jijini na kulala kabla ya kurauka mapema kuendelea na safari yako ya masaa mawili hadi Nairobi.

Niliamua kukaa majuma mawili kijijini kwetu licha ya kibaridi kikali sana cha mwezi wa saba. Kwa miaka mingi sana sijapata fursa ya kukaa kijijini na hasa nyumba nilimolelewa. Kipindi cha majuma mawili kingefaa kupiga gumzo na mamangu mpendwa. Kabla ya kuenlekea Cape Town kwa kongamno langu nilikuwa nimetua Kenya kwa wiki moja kumjulia hali mama na ndugu zangu. Nilifurahi kuona afya yake imeboreka sana tangu mwezi wa Januari nilipomwona. Sasa nilikuwa na fursa mwafaka kusema mengi ambayo hatujapata kuongea ana kwa ana. Ingawa kila mara humpigia simu kumjulia hali na kupata mawaidha ya hiki na kile hatujapata fursa ya moja kwa moja kwa muda mrefu.

Kwa mara ya kwanza alipata kunielezea mengi ya ujana wake na maisha ya familia yake kutoka ukoloni hadi baada ya uhuru. Kumhusu ndugu yake aliyejitolea kupigania uhuru kama Mau Mau na alivyopata kuyapoteza maisha yake. Tulizumngumza mengi kuhusu familia yetu, jinsi walivyokutana na marehemu baba yetu na kuhusu maisha yao kabla wajaliwe kufungua mimba na walivyotulea sis wanao wafikao zaid ya kumi wakiwemo mapacha wawili. Tulizungumza ya malezi na nilivyoshangazwa na uwezo wao mkubwa wa kuwalea watoto wengi na walipojaliwa kusoma sana na kuweza kuhudumia jamii katika nyadhafa mbalimbali katika miji na mataifa ya karibu na hata ughaibuni. Miye ninao wawili na mzigo si mwepesi licha ya kazi yangu ya uprofesa. Mbali na mazungumzo nilipata fursa ya kufanya kazi nyumbani nilizofanya nikiwa mtoto na mengineo mengi.

Siku ya mwisho kule kijijini kabla ya kuondoka kurudi ughaibuni ninakoishi, nilijitolea kumpikia mama supu ya mifupa ya ng'ombe na nyama karanga. Baridi ya Julai ilikuwa imekolea na umri wake wa miaka takriban 80 aliathiriwa viungo vya mikono. Siku hiyo akasisitiza tule pamoja na dada zake, yaani shangazi zangu wapenda. Wakaja na kunilitea zawadi za majani chai kusudi tufurahie chai ya kwetu tukiwa ughaibuni. Tukapiga gumza na kufurahi sana pamoja. Kesho yake nikamuaga mamangu na kuelekea Nairobi kuchukua ndege ya kunirejesha huku ughaibuni.

Sikujua hiyo ingekuwa siku ya mwisho kumkumbatia na kusema na mamangu. Ilikuwa mwezi wa tisa nilipoipokea simu ya majonzi kutoka kwa kakangu. Takriban miezi miwili tangu safari yangu ya Cape Town zikiwemo wiki mbili zilizosheheni mapenzi ya mama mapendwa pale kijijini nilikozaliwa.

Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page