Trump, Idi Amin, Ferguson, na Katrina
- Mungai Mutonya
- Apr 3, 2016
- 2 min read

Katika miaka ya hivi karibuni nchi ya Amerika imekumbwa na matatizo ambayo yamewadhihirishia wengi ambao hawajahi kuitembelea nchi hiyo kuwa mambo sivyo kama Hollywood inavyoonyesha. Taswira ya Amerika ya majumba marefu yenye nakshi, magari makubwa, barabara pana zilizojengwa kwa ustadi mkubwa wa kihandisi, nyumba za kifahari zenye bustani za kuvutia macho, inadidimia kwenye fikra za wengi. Aidha Amerika ya mabingwa kama vile Lebron James, Tiger Woods, Serena Williams, Beyonce, Jay Z, inagubikwa na taswira za Donald Trump, Trayvon Martin, Michael Brown, mafuriko ya Katrina, vurugu mjini Ferguson, na maandamano ya kutetea haki.
Dunia imeshuhudia kuwa chini ya taswira ya utajiri na ufanisi mkubwa kuna pia umaskini, ubaguzi wa rangi, kutokuwa sawa, na maovu mengine ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Mafuriko yaliyoukumba mji maarufu wa New Orleans kufuatia kimbunga kikubwa cha Katrina, mwaka 2005, yaliifungulia dunia pazia kuuona umaskini na hali ya kutokuwa sawa nchini Amerika.Weusi wengi walipoteza makazi yao na kwa siku nyingi wakawa wanaishi kwenye kiwanja cha mpira katika hali duni. Wamarekani kuishi bila maji, chakula, vyoo vya kutosha, matibabu, na hata wengi kufa bila kupewa huduma kuliwashangaza wengi. Ilifikia hata nchi kama Cuba na baadhi ya nchi za Afrika kujitolea kuwasaidia Wamerikani Weusi wa New Orleans walionekana kupuuzwa na serikali yao. Bila shaka serikali ya George W. Bush haikukubali msaada huo. Lakini taswira ya Amerika kuwa paradiso ilipata pigo kubwa.

Baadaye kukatokea msururu wa kesi za vijana weusi kupigwa risasi na kuuawa kiholela na polisi wazungu. Kesi ya Trayvon Martin, kijana mweusi aliyeuawa na mlinzi mzungu, George Zimmerman, kwa kushukiwa kuwa anakusudia kutenda uhalifu ilionyesha mshikamano wa polisi na mahakama katika njama za kuwatisha na kuwakandamiza watu weusi, hususan vijana. Mahakama ya Florida iliamua kuwa aliyemuua Travyon Martin hakuwa na hatia na kwa hivyo Zimmerman akaachiliwa huru. Maandamano yakatanda sehemu nyingi waandamanaji wakidai haki. Licha ya hayo, vijana wengine zaidi wamepigwa risasi na kuuawa na polisi wazungu Marekani. Mtindo wa polisi kuachiliwa na mahakama unaendelea. Lakini alipouawa Michael Brown kwa kushukiwa aliiba peremende katika duka moja mjini Ferguson, ikawa hamkani si shwari tena. Maandamano yaligeuka mapambano makali baina ya raia na polisi. Dunia ilishuhudia mapigano na maandamano hayo yaliyotangazwa kote duniani. Hali duni ya makaazi wamaoishi maskini wa Amerika, hususan watu weusi, ikathihirika bayana na ulimwengu.

Sasa kwenye kampeni za kugombea uraisi hapa Amerika, sura ya migawanyiko ya kijamii na kirangi inawakilishwa mgombea kiti cha urais, tajiri na domokaya Donald Trump. Matamshi na vitendo vyake pamoja na vya wafuasi wake -- wengi wao wakiwa ni wazungu -- vinaonyesha wazi zaidi pengo hili la kijamii. Si ajabu kuwa mcheshi mashuhuri wa televisheni nchini Amerika, Trevor Noah, anamlinganisha Donald Trump na Field Marshall Alhaji Professor Idi Amin Dada wa Uganda. Itakumbukwa Amin alipenda kujisifu sana na kujitangaza kuwa ana vipawa vingi, vikiwemo kuweza kusema na Mungu, lakini alijulikana kuwa zuzu. Kutokana na ujinga wake na kutoielewa vyema dunia, Amin alisababisha vifo vya Waganda wengi sana.
Hollywood na vyombo vya habari vimegubika dunia kuhusu uhalisi wa jamii ya Marekani. Nyumba nzuri si mlango, walinena wahenga, fungua uingie. Aidha, usipoziba ufa utajenga ukuta.
תגובות