top of page

Wasiwasi Katika Chuo Kikuu


Washington University in St. Louis Shooting

Leo alasiri niliupokea ujumbe wa dharura kwenye simu yangu ya mkononi "Mwalimu uko sawa?" Sikuwa nimeujibu ujumbe huo wa pili ulipoingia "Umesikia kilichotokea?" Nilishtuka. Nilikuwa nimetoka darasani dakika chache tu na sikuona cha mno ila wanafunzi na wahadhiri wenzangu wakiwa kwenye shughuli za kawaida.


Lakini nilikumbuka kusikia king'ora cha magari ya polisi -- jambo ambalo si geni hasa wakati mvua inapoanguka. Jamaa huteleza na kuanguka. Wanafunzi wenye kuendesha baiskeli hutatizwa na miavuli na mara hugongana na wanaotembea miguu. Lakini ujumbe ulikuwa na dharura ya kipekee. "Kumetokea nini? wapi?" Nikajibu kwa upesi huku nikiwasha kompyuta kuzisoma baruapepe. Kuchungulia nje ya dirisha langu nikashangaa hakukuwa na watu wanaotembea kwenye vinjia vya chuo kikuu. Ni saa saba unusu na kawaida shamrashamra za kutafuta chamchana huwa zimeshika kasi. Kuangalia baruapepe nikaona ujumbe wa dharura kutoka chuo kikuu:


"Onyo!!! Kumetokea ufyatuliana wa risasi karibu na chuo kikuu. Alifyatua risasi amekimbia kuelekea chuoni. Polisi wanamsaka. Jifungieni hadi tutakapowaarifu."


Nikaufunga mlango wa ofisi. Ujumbe mfupi ukaingia. "Mwalimu, kuna mtu hatari chuoni. Jifungie ofisini. Sisi tumejifungia darasani mwetu. Wanasema leo ni siku ya kuadhimisha mashambulizi ya shule ya Columbine." Nikamtuliza mwanafunzi ingawa nilikuwa na wasiwasi pia. Nikafuatilia habari kwenye mtandao wa kijamii kama Twitter na Yik Yak.


Dakika thelathini baadaye tukapata ujumbe kuwa hali ni shwari na turejee shughuli za kawaida. Habari zilieleza kuwa kisa na maana cha vurugu hili lote ni kutoheshimiana barabarani. Dereva mmoja alikasirishwa na mwingine. Akatoa bastola na kumjeruhi abiria wa gari la pili aliyekuwa mfanyakazi wa chuo kikuu. Kisa kilitokea karibu sana na chuo kikuu ndiposa hatua za dharura zikachukuliwa.


Visa vya ufyatuliana risasi katika vituo vya elimu na kazini vimezidi sana nchini Marekani. Itakumbukwa kwamba mwaka 1999 wanafunzi wawili waliwaua wenzao kumi na wawili na mwalimu mmoja katika shule ya sekondari ya Columbine, jimbo la Colorado. Mwaka 2012, watoto wadogo ishirini waliuawa shuleni sandy Hook. Walikuwa watoto wenye umri wa katika ya miaka 6-7. Mauaji mengine yametokea kwenye sinema, vituo vya kijeshi, na kwingineko.


Suala la umilikaji wa bunduki ni suala nyeti katika mvutano wa kisiasa baina ya vyama vya Demokrat na Republikan. Wakati wanademokrat wanataka kupunguza ununuzi na umilikaji wa bunduki hatari, wapinzani wao wanadai ni haki ya kikatiba aliopewa raia kumiliki bunduki yoyote na kwa wingi anaopenda.


Wasiwasi hautaisha miongoni mwa raia hadi suala hili litakapotatuliwa. Huzuni ni kuwa kuna majimbo yaliyopitisha sheria kuruhusu wanafunzi na walimu kuleta bunduki chuoni na darasani. Hatari kubwa!!


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic
bottom of page