top of page

Trump na Biden: Handisheki Au BBI Marekani?

Updated: Jan 27, 2021


Hatimaye Donald Trump ameondoka Ikulu ya White House. Hakutaka kuondoka lakini kauli ilikuwa ishakatwa na hakuwa na lingine ila kugura. Hakudhani angeng’atuka uongozini pasipo na sherehe kabambe ya kumuaga ikiwemo na gwaride, fataki, nderemo na halaiki ya wafuasi. Mambo hayakuwa alivyotarajia. Jahazi lake halikuabiri hadi bandari alilopanga kutia nanga. Alipanda ngazi na - pasipotokea muujiza wa handisheki na BBI kama ilivyotokea nchini Kenya - atashuka na kuwa mshindani anayekubali kushindwa.

Takribani miezi mitatu baada ya kushindwa kwa zaidi ya kura milioni 4, Trump amejaribu uganga wa kila sampuli kusalia madarakani: si ushawishi, si shinikizo za kisiasa, si mahakama, na hata uchochezi, yote yameshindikana. Kama ilivyo kwa wanaoonja asali ya mamlaka ya ubunge, useneta, umama kaunti, ugavana, au hata urais wasipuuze hekima ya wahenga inayowashauri kuwa “ajidhaniye amesimama aangalie asianguke.” Trump alidhani amesimama kidete ana akaichovya asali ya uongozi na sifa ambatanishi akasahau kuwa sifa humfanya mwema mwema zaidi na mbaya mbaya zaidi. Akazua taharuki na hali ya mshikemshike kote nchini kwa kung’ang’ania mamlaka licha ya kushindwa kwenye uchaguzi. Taharuki iliyotanda hata nje ya mipaka ya Marekani kwa sababu nchi hii ikichefua, nchini zingine hupata korona.

Ndiyo maana usiku wa kuamkia tarehe ishirini ya mwezi wa Januari mwaka huu mpya, sikupata usingizi wa kutosha. Alfajiri na mapema nilirauka na kuiwasha runinga kushuhudia yatakayojiri. Picha zilizopeperushwa za wanajeshi wakipiga doria barabara tupu za jiji kuu la Washington DC ziliniongezea taharuki. Nilikumba kila nitembeleapo jiji hili kuna misongamano ya magari na watu lakini leo ningefanya mazoezi yangu ya asubuhi ya kunyoosha mwili barabarani bila shida. Fauka ya hayo, taharuki yangu ilizidishwa na kumbukumbu za wanajeshi jijini Nairobi palipotokea mapinduzi ya 1982, wakati wa harakati za vyama vingi, na hata maandamano yaliyofuata baada ya kuawa kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya nje: Robert Ouko.

Trump amezifanya papara zisizopata kuonekana Marekani na yumkini angeweza kukataa kung’atuka ama akatumia madaraka ya urais kuivuruga sherehe ya kuapishwa kwake Joe Biden na Kamala Harris. Tayari alikuwa amewahamasisha wafuasi wake na uwongo kuwa alishinda uchaguzi nayo Deep State ikampokonya ushindi. Hata maneno yake yakasababisha waivamie Bunge la Congress kusudi wavuruge uratibishaji wa matokeo ya uchaguzi. Lakini akasahau kuwa hakuna mume wa waume na nzige hawana mfalme.

Sijui aliwachochea wafuasi alikusudia nini lakini angalisoma kuhusu shujaa Kinjeketile Ngwale aliyewaongoza Watanganyika kwenye vita vya Maji Maji dhidi ya mkoloni, angalipata ushauri kuhusu maneno tuyasemao tukiwa viongozi. Mwanatamthilia mashuhur Ebrahim Hussein aliyenasa fikra za shujaa huyu kwenye tamthilia iitwayo Kinjeketile, “Binadamu huzaa neno, neno hushika nguvu, likawa kubwa, kubwa likamshinda binadamu kwa ukubwa na nguvu. Likamuangusha.” Ni rahisi sana kwa kiongozi kuwachochea wafuasi wake wakajawa na hamaki wakitaka kumtetea kiongozi wao ‘anayekandamizwa.’ Pengine alikusudia kufuata mfano wake Raila Odinga na Miguna Miguna aapishwe mbele ya wafuasi wake halafu baada yeye na Biden wawe handisheki na BBI huku Kamala Harris akitemwa.

Runinga ilizijeresha ndoto zangu jijini Washington DC kuonyesha ndege ya kumsafirisha rais wa Marekani iitwayo “Air Force One” ikitokomea upeo wa macho kumpeleka Trump na aila yake Florida watakapoishi. Lazima wawahi huko kabla ya saa sita mchana wakati wadhifa wa uraisi utafikia kikomo. Hatimaye rais mpya, Joe Biden, akaapishwa na kuchukua mamlaka rasmi.

Wachanganuzi wa masiala ya kisiasa watautadhamini utawala wa Donald Trump kwa jicho pevu wakiulinganisha na ule wa marais wengine arobaini na wanne wa Marekani waliomtangulia. Kabla ya hapo ukaguzi sahili wa miaka minne ya utawala wa Trump unawapa mafunzo na tahadhari viongozi popote walipo.

Kiburi na majuto. Trump alitumia kiburi, matusi, dharau, na kujitapa kama zana na kukabaliana na wapinzani wake. Twakumbuka alivyowatusi na kuwadhalilisha viongozi wengi na kuwapachika majina kama vile “Hillary mkora,” “Mbilikimo Rubio,” “Bernie kichaa,” “ fulani wa fulani feki” na mengineo mengi. Angalijua ulimi unauma kuliko meno asingalijikwaa ulimi jinsi alivyofanya. Matusi yake yaliwaudhi wengi na kuwadhalilisha viongozi wenzake na hapo basi kapoteza kura nyingi ambazo zingemhakikishia ushindi. Alionekana kuwa na uhasama mkubwa dhidi ya wanawake na watu weusi.

Kweli iliyo uchungu, si uwongo ulio mtamu. Yaani afadhali kuambiwa ukweli mchungu kuliko kuhadaiwa na uwongo mtamu. Aidha uongo ulikithiri katika utawala wa Trump. Akasahau ushauri wa Bob Marley aliyetahadharisha kuwa unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa muda fulani lakini kamwe huwezi kuwadanganya watu wote daima. Wanasiasa wengine wanapenda kutumia uongo kujipatia manufaa ya muda mfupi lakini waongo wanapaswa wawe na kumbukumbu nzuri kwani siku moja ukweli utadhihirika. Janga la Korona lilipozidi kuenea na uchumi kuzorota, Trump aliendelea na uwongo wake kuwa kila kitu ki shwari, gonjwa litatokomea na uchumi unastawi kuliko awali. Huku mashinani hali ilikuwa ngumu na wengi walijua bayana asemayo ni uwongo. Lakini alijizingira na matapeli wa kisiasa waliomsifu na kumpatia uwongo kila mara. Kiongozi afaa authamini ukweli mchungu.

Sheria nayo haijui nguvu na haina kwao. Licha ya kuwa kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kijeshi, kiuchumi na kisiasa Trump haruhusiwi kamwe kukiuka sharia za nchi. Kiapo cha urais kinamlazimu awe mlinzi na mtetezi wa katiba, serikali, na sheria zote zinazohakikisha utawala mwema na haki. Sheria hukata pande zote na alipovunja sheria Trump aliadhibiwa mara ya kwanza na Bunge la Congress. Kwa mujibu wa sheria uraisi wake ulipatwa tope la kihistoria kama adhabu ya upotovu wake. Lakini alipoamrisha wafuasi wake waivamie Bunge kwa nia ya kubaki mamlakini kwa njia isiyo halali, hapo alicheza na simba na kumtia mkono kinywani. Sheria itamwandama na kumkumbusha kuwa demokrasia husimama kwenye nguzo za sheria. Dhuluma huanza pale sheria iishapo. Avumaye bahari papa kumbe sheria ndiye papa mkuu. Alijaribu kuyavuka maji asiyoweza kuyaoga.

Siku hiyo nilishinda mbele ya runinga nikishuhudia ushindi wa sheria katika nchi yenye demokrasia iliyokomaa. Demokrasia mapinduzi ya serikali yakiongozwa na raisi aliyeshindwa uchaguzi. Hata hivyo, licha ya nguvu alizopewa za kisiasa na kijeshi bado akabanwa na sheria. Nilihofia kungekuwa na vita baina ya mirengo miwili ya kisiasa na nilikuwa tayari kuihamisha jamaa yangu maji yakizidi unga.

Baada ya mbwembwe, vitisho, njama za kichochezi dhidi ya serikali aliyoiongoza, Trump hakuwa na lingine ila kumeza vidonge vya ushindi na kugura Ikulu. Naye Joe Biden na Kamala Harris wameapishwa rasmi kuchukua hatamu za uongozi nchini Marekani.

Nilivutiwa na jinsi hali ilivyorejea shwari na taharuki kuondoka mara tu wazalendo walipoamua amani nchini ni muhimu kuliko ustawi wa kiongozi mmoja mwenye kiburi na ubinafsi. Lakini wanasema kwenye uwanja wa kisiasa hakuna maadui wa kudumu ila maslahi ya kudumu. Je, inawezekana kukawa na handisheki na BBI hapa Marekani?

Comentarios


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic

FOLLOW ME

  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • c-youtube

© 2023 by Samanta Jonse. Proudly created with Wix.com

bottom of page