top of page

Mtoto Asiye Na Jina

Prince William and Kate Milton

Vipindi vya televisheni vinapeperusha matangazo ya moja kwa moja kutoka hospitali ya St. Mary’s mjini London. Wanahabari wamekuwa hapo tangu Julai 1 wakisubiri kuzaliwa kwa mtoto. Wameufuata kwa makini mwendo wa mama mjamzito Kate na mumewe William. Tunamiminiwa historia ya kuvutia ya familia hiyo. Ci eN eN inatangaza “tunakatiza kipindi chetu kuhusu afya yako kuwaleteeni habari kemkem kutoka London: Kate amefika hospitalini. Twende moja kwa moja hadi London kwa mtangazaji wetu Cinderella Snow White” Baadaye habari zingine motomoto zinaripotiwa “mtoto amezaliwa,” “mizinga 41 inafyatuliwa” kumkaribisha mtoto atakayekuwa mfalme pengine mwaka wa 2079.


Wakati huohuo, katika hospitali ya Pumwani, jijini Nairobi, amezaliwa mtoto. Wazazi Kate Akinyi na William Wanjohi wanampatia mtoto jina Tumaini. Wakitumaini mtoto wao atakuwa na maisha mema kushinda yao. William akitumaini atapata kibarua cha pili huko Industrial Area ili aweze kupata mapeni ya kutosha kununua chakula na kulipa nyumba. Kate anatumaini hatapata matatizo yoyote ya kiafya ili arudi haraka kwenye kibanda chake cha kuuza mboga mtaani. Lau sivyo pesa walizoweka za kununua mahitaji ya mtoto zitakwisha. Bahati ni kuwa serikali imeondoa gharama kwa akina mama wanaojifungua kwenye hospitali za serikali. Nje ya hospitali ya Pumwani milio mitatu ya bunduki inasikika. Polisi wanafiatuliana risasi na majambazi. Hakuna Kei Ti eN, eN Ti Vi, wala Kei Bi Ci kuripoti kuzaliwa kwa mtoto huyu ambaye pengine atakuwa mwanasayansi shupavu.

Mjini Aleppo katika nchi ya Syria, Kate Kalilah na William Wahid wamempata mtoto. Shangazi yake amemsaidia Kate kujifungua nyumbani kwa sababu hakuna hospitali zilizobaki. Zote zimebomolewa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kate hana furaha kwa kuwa hajui kama mume wake atarudi nyumbani kumwona mtoto wao kifungua mimba. Willliam alijiunga na wanaume wenzake kupigana vita vya kuulinda mji wao. Kate hajapata habari kutoka kwa mumewe kwa wiki tatu sasa. Nje mizinga inafyatuliwa, risasi zinafyatuliwa, na mabomu kulipuka. Hakuna wanahabari wa Ci eN eN, Bi Bi C, na wengineo kutangaza maafa yanaondelea. Wote wamepiga kambi nje ya hospitali ya St. Mary’s, mjini London. Wakisubiri habari muhimu zaidi dunia: kuzaliwa kwa mtoto.


Aidha, katika hospitali moja hapa Marekani, iwe mjini Boston, St. Louis, Houston, ama Atlanta, amezaliwa mtoto Mkenya. Yeye ni Mkenya mwanadiaspora na pia ana uraia wa Marekani. Wazazi wake watafurahi na kushangilia. Ilivyo kawaida akina mama Wakenya watamtembelea hosptalini na nyumbani na kumpelekea uji, njahi, chapati, na zawaidi zingine. Baadaye atapelekwa kanisa za Kikenya kubatizwa. Atapelekwa Kenya kumsalimia cucu, babu, wajomba, na mashangazi. Atalelewa na mama moja Mkenya aliyefika kuwasalimia wanawe wanaoishi Ughaibuni. Mama mtu atafanya kibarua cha kulea watoto kusudi apate tikiti ya kurudi Jamhuri. Panapo majaliwa mtoto atasomea huku Marekani, atahitimu vyuo vikuu, atapata kazi nzuri, na baadaye awe mtu wa kuchangia ustawi wa watu wote duniani.


Vilevile huko Mogadishu, kambi za wakimbizi za Gaza Strip, kwenye makazi duni ya Brasilia, Chicago, Mathare, Soweto, Mumbai, na Manila, mamiloni ya watoto wamezaliwa leo. Wazazi wao watakuwa na upendo na matumaini kama ya wazazi Kate na Williams wa Windsor, London. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa maisha yao hayatafuata mkondo mmoja.


Sitaki kukitia kitumbua mchanga ama kuukatiza uhondo wa karamu hii iliyoandaliwa na wanahabari ya kusherehekea kuzaliwa mwana mfalme. Lakini ni muhimu kwa wanahabari kuyazingatia mambo mengine yanayoendelea kote duniani. Ni muhimu tufikirie hali ya watoto duniani. Hasa watoto wanaoishi maisha duni yenye umaskini, vita, na magonjwa. Kwa mujibu wa mashirika kama UNICEF na WHO, zaidi ya watoto milioni 6 wanakufa kabla ya kufikisha miaka 5. Wengi wao wakizaliwa katika nchi za Kiafrika na zile zenye mapato madogo. Ajabu ni kuwa vifo vya watoto wengi vinaweza kuepukwa. Wengi wanakufa kwa ukosefu wa chakula, maji safi, na madawa. Pia ukosefu wa habari muhimu na elimu huchangia. Malaria, nyiumonia, na kuhara ni baadhi na magonjwa mengine yanayowaua watoto hawa.

Nchi ya Kenya inasifiwa kwa kupiga hatua za kuzuia vifo vya watoto wachanga. Serikali imewezesha raia kupata huduma ya afya bila malipo. Akina mama wajawazito wakijifungua hospitalini bila malipo, kama serikali ilivyoamuru hivi majuzi, maisha ya mama na mtoto hayatakuwa hatarini. Wenye ujuzi wa afya wanasema siku za kwanza 28 ndizo zenye hatari kubwa baada ya mtoto kuzaliwa. Pia mtoto akizaliwa hospitalini atapata chanjo za kukinga magonjwa na hata ushauri wa kiafya. Pengine hata watapewa nyavu za bure za kuzuia mbu na hivyo basi kujiepusha na ugonjwa wa malaria. Vilevile kuna wakunga (midwives) vijijini ambao wanawazalisha mama wajawazito vijijini. Wakunga hao wanafanya kazi muhimu sana. Pengine serikali inahitaji kuwatambua na kuwalipa kama njia moja ya kuendeleza afya vijijini. Kumbuka methali isemayo kuwa tusitukane wakunga na uzazi ungalipo.


Wengi wenye kuyajali maslahi ya watoto wote dunia wanaendelea kusaidia ili kila mtoto apate haki yake ya kuishi na kukua kuwa mtu mzima. Akina Bill Gates na Bill Clinton wanatoa michango mikubwa ya kuwapa watoto chanjo na kupambana na magonjwa mengi. Makanisa na watu binafsi husaidia watoto mayatima na wale maskini zaidi kupata maisha bora zaidi. Wanasiasa wenye maono (vision) mema wanahimiza sera za kuendeleza kilimo, afya bora, na amani ili watoto wakue katika mazingira yafaayo. Kila mtoto ana haki ya kuishi. Hakuomba azaliwe kwenye mazingira ya kifalme ama yenye umaskini. Ni kiumbe wa Mungu na huenda akayaleta mabadiliko yatakayobadilisha ulimwengu.


Tusisahau kuwa zaidi ya karne mbili zilizopita, wazazi wawili walifika mjini lakini hawakuweza kupata nafasi kwenye hoteli. Hawakuweza kufika hospitalini ili mama ajifungue. Hapakuwa na wanahabari kushangilia kuzaliwa kwa mtoto huyu. Mtoto alizaliwa katika hali duni sana: zizi la ng’ombe. Lakini mtoto huyo akaibuka kuwa mtetezi mkubwa wa watu duni na mwokozi wa dunia: Yesu Kristo. Wanahabari wa siku hizi wangelikuweko Yerusalemu siku hiyo hawangetumia hata dakika moja kuyajali yanayoendelea zizini alikozaliwa Yesu. Wangekuwa wamepiga kambi kasri kuu wakisubiri kuzaliwa mtoto wa Kaisari.

Hongera kwa wazazi wote duniani wanaosherekea kuzaliwa kwa mtoto wao mpendwa. Kama mamangu anavyopenda kusema, “mtoto anyonye kwa mashavu yote mawili.”

 
 
 

Comentarios


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic

FOLLOW ME

  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • c-youtube

© 2023 by Samanta Jonse. Proudly created with Wix.com

bottom of page