top of page

Kichaa cha Mwezi wa Machi: Michezo


Mwezi wa Machi umewadia nayo ngoma ya mchezo wa kikapu imeshika kasi. Mashindano ya kitaifa baina ya timu 64 za vyuo vikuu itaanza hivi karibuni. Timu hizo ni zile zilizofuzu kushindana kwenye mashindano ya kitaifa baada ya kuibuka na matokeo mema katika ligi zao. Kila chuo kikuu kinapenda timu ishiriki kwenye mashindano ya kitaifa kwa sababu nyingi. Muhimu zaidi ni kuwa hii huwa ni fursa murwa ya kijitangaza. Timu zinazofanya vyema hupata kujulikana zaidi na wanafunzi wapya wakataka kujiunga navyo. Pia timu zinazoshinda hupata fursa nzuri ya kuwasajili wachezaji wapya wenye talanta za mchezo huu. Aidha, shule hulipwa kiasi fulani za hela za utangazaji wa michezo hii kwenye televisheni. Sijataja fahari ya wanafunzi kwa chuo chao na timu zao. Kuna miamba ya michezo hii ambao hutarajiwa kushinda au kufanya vizuri sana kila mwaka. Timu za vyuo kama vile Duke, North Carolina, Kansas, Michigan State, na nyinginezo. Fahari yangu ni kwa chuo nilichosomea shahada yangu ya udaktari: Michigan State au kwa jina la utani "Spartans". Timu yetu imekuwa ikifanya vizuri sana tangu kocha Tim Izzo achukue hatamu za uongozi. Tumewahi kuwa mabingwa wa kitaifa mwaka wa 2000 na pia mwaka wa 1979 wakati Magic Johnson alipokuwa mwanafunzi. Miaka ya hivi karibuni tumefikia nusu na hata robo fainali.



Kichaa cha mashindano haya ya kitaifa ni kamari ambayo Wamarekani wengi wanashiriki. Kabla ya mashindano kuanza, mashabiki wanabashiri timu zipi zitashinda kuanzia mchujo hadi ubingwa. Wale watakaobashiri vyema hupata donge nono katika kamari inayochezwa baina ya wanafamilia, marafiki, wafanyakazi, au kwenye vikundi mbalimbali kwenye mtandao. Ni biashara kubwa kwa wenye televisheni, vilabu vya pombe, magazeti, kasino, mikahawa, vyuo vikuu, mashabiki, na kadhalika. Hata Rais Obama hushiriki katika shamrashamra ya kubashiri mwelekeo wa mashindano. Tajiri Warren Buffet aliahidi kulipa dola bilioni moja kwa yeyote atakayebashiri asilimia 100 bila kukosea. Hakuna aliyeshinda bilioni za Buffet.


Timu yangu ya Spartans inatarajiwa kufanya vyema chini wa unahodha wake Denzel Valentine na mlenga shabaha hodari, Forbes. Twende Spartans!

 
 
 

Commenti


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic

FOLLOW ME

  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • c-youtube

© 2023 by Samanta Jonse. Proudly created with Wix.com

bottom of page