Kichaa Mwezi wa Machi: Uchaguzi
- Mungai Mutonya
- Mar 1, 2016
- 1 min read

Karibu mwezi wa Machi! Leo tunaukaribisha mwezi kwa msisimko wa uchaguzi wa mchujo wa vyama vya Democrats and Republican. Mbali na kuwa nilisomea elimu ya siasa (Political Science) na Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, nakashiriki kwenye siasa za kupinga siasa za chama kimoja na utawala wa mabavu wa Daniel Arap Moi, ninakiri kuwa siasa huchangamsha nafsi yangu. Hii leo basi, tarehe mosi mwezi wa Machi, tutashuhudia kinyang'anyiro chenye uhondo. Tutajua iwapo kichaa cha Donald Trump kitapewa nguvu zaidi au kitadidimishwa. Pia tutagundua iwapo Hillary Clinton atachukua hatua muhimu kuwa mwanamke wa kwanza kupewa tiketi ya kuongoza chama cha Democrat kwenye uchaguzi mkuu na pengine kuwa raisi wa kwanza mwanamke katika historia ya Marekani. Ni ajabu kuwa nchi ya Marekani yenye kudai inazitetea haki za wanawake kuliko nchi nyingine ye yote haijamchagua mwanamke hata mmoja kuwa raisi. Tukumbuke Marekani ilipata uhuru mwaka wa 1776. Nchini nyingi changa, zikiwemo Liberia, Zambia, na Central Africa Republic, tayari zishachagua wanawake kuwaongoza. Brazil, Uyahudi, Uhindi, Uingereza, Taiwan, Ujerumani, Argentina, na zinginezo zishawachagua viongozi wanawake. Je, Hillary Clinton atabadilisha taswira hii ya Marekani?

Lakini inaonekana wazungu wengi wameendelea kuchukizwa na uchaguzi wa Rais Baraka Obama, mweusi wa kwanza kushikiria hatamu hiyo. Ikumbukwe Wamerkani weusi walikuwa chini ya utumwa wa wazungu kwa miaka mingi na hadi wa leo kuna wazungu, hasa wanaume, ambao wanaamini nchi ya Marekani ni yao na wanafaa kushikilia nguvu zote za kisiasa, kiuchumi, kidini, magazetini, na kwingineko. Si ajabu ukaona Donald Trump anaendelea kupata kura licha ya matamshi dhidi ya kichaa dhidi ya Waislamu, wahamiaji, na wanawake. Haya tusibiri matokeo ya kidubwedubwe hiki leo jioni.
コメント