top of page

Barua ya Mheshimiwa Mwizi wa Miwa Mtarajiwa

Idara ya Umaskini na Waathiriwa wa Ghasia

Wizara ya Mipango Maalum

Jamhuri ya Kenya


Bwana Mdosi Mkuu,


KUH: BARUA YA KUJIUZULU


Mintarafu na katiba yetu mpya, wengi wamejiuzulu nyadhifa zao serikalini ili kuwania viti tofauti kwenye uchaguzi mkuu ujao. Mimi sitoachwa nyuma.


Ninaandika kukuarifu kuwa nimejiuzulu cheo changu mara moja. Ninarudi kwetu kupigania kiti cha ubunge cha eneobunge la Mashinani Kusini. Kwa kuufuata mfano wa watarajiwa wengine mimi pia nimechapisha kitabu kiitachwo Mitumba – nisogee, kisura, nisogee!


Kazi ya ofisini imenichosha. Nimechoka kurauka mapema ili niepuke misongamano ya magari kuingia jijini. Nimesinywa kusubiri masaa ya ofisini nikiwa kanisani huku nalisoma gazeti la jana. Ninaudhika kuzururazura jijini, kichokoa meno kikiwa kinywani huku tumbo linanguruma njaa wakati mwezi uko kona. Huku wimbo wa Gabriel Omollo, Lunchtime, ukiniongoa.


Napungia mkono wa buriani chai mbovu ofisini, masengenyo ofisini, ukiritimba, na maisha ya kuhudumia jamii. Ninataka kuyajali maisha yangu binafsi na yale ya familia yangu. Ninataka kuwa mbunge wa eneo la Mashinani Kusini.


Baada ya kuihudumia serikali kwa miaka ishirini na saba, nimeamua huu ni wakati ufaao kujitosha kwenye uwanja wa siasa. Nimeyatathimini maisha yangu na ya famila yangu na kufikia uamuzi huu. Aidha, wapiga kura wa Mashinani Kusini, hususan jamaa zangu, wamenisihi niliokoe jahazi kwa kuwa mbunge wao. Wanaamini, na ninakubaliana nao, kuwa nitakuwa mbunge bora kuliko mwakilishi wetu.


Kwanza, nikiwa mbunge nitaweza kuyashughuikia maslahi yangu na ya jamaa yangu vyema zaidi. Mke wangu ataweza kuanzisha kampuni ya ujenzi na kuzipata kadarasi zenye donge nono katika eneobunge langu. Wanangu watazipata kazi nzuri kwenye kampuni zitakazodhamini miswada yangu bungeni. Wengine watapata udhamini wa kimasomo kwenye mataifa ya kigeni nikiwasaidia mabalozi wao kupata siri za serikali yetu au kupata kadarasi zenye donge nono nchini.


Pili, nikiwa mbunge nitashirikiana na wenzangu kujiamulia mshahara na marupurupu. Siijui taasisi nyingine yenye uwezo huu lakini nitafurahia kushiriki kikamilifu kwenye miswada ya sampuli hii bungeni. Fauka ya hayo, sitalipa kodi ya mapato. Fikiria hayo, Mdosi, sitalipa kodi ya mapato!! Kwa miaka yote hii niliyoifanyia serikali kazi na kuhudumia umma kwa uzalendo, mshahara na marupurupu yangu ni ya kusikitisha. Kodi nayo imenivunja mgongo.


Tatu, nitafanya kazi siku chache kwa mwaka na kulipwa mshahara mnono zaidi kuliko mbunge ye yote duniani. Kufanya kazi kwa siku tatu tu za wiki kwa miaka sita tu ya mwaka huku ninalipwa mamilioni ya shilingi. Zaidi ya hayo, umeiona fenicha na nakshi ya bunge mpya? Lo salala! Ungedhani ni jumba la kifalme kule Uingereza. Na tulitumia mamilioni mangapi kununua mikeka, viti, vipasa sauti, na madoido mengine?


Yumkini ni muhimu kivikalia viti vya kistarehe hivyo tunapoijadili miradi ya kuumaliza umaskini nchini. Pengine kuvikalia viti kama hivyo kutatuwezesha kubaini jinsi tutakavyoweza kuwapatia makazi mema waadhiliwa wa vurugu la mwaka 2007.


Ama pia kutuwezesha kugundua jinsi tutawapa makazi bora wakazi wa maeneo ya madongoporomoko wa Sinai, Mathare, Kibera, na kwingineko. Ama hata kuwapatia vijana wetu kazi. Sina shaka viti hivyo vitatuwezesha kujadili maswala muhimu ya kitaifa kama vile kujiongezea mishahara na kutolipa ushuru.


Nne, nani asiyependa kudekezwa na kuitwa "Mwizi wa Miwa"? Ni nani asiyekuwa na ari –baada ya kulipwa mshahara mnono na kudekezwa -- ya kubweka bungeni akimtetea kiongozi wa chama chake licha ya ukweli ujulikanao kuwa ni kiongozi mfisadi na mkosa utu.


Nani asiyekuwa na utu wa kumkashifu kiongozi wa chama kingine licha ya ukweli kuwa anautumikia umma kwa udhati wa moyo na uzalendo usiokuwa na dosari? Ninadhani kushangilia sarakasi hii ya kitaifa kunastahili kuvikalia viti vya kistarehe na kulipwa mishahara minono. Waadhiriwa wa vurugu baada ya vurugu wanastahiki kuishi hemani.


Mdosi, hii kazi ya kuwahudumia wakulima, waadhiriwa wa ghasia za uchaguzi, na vijana hapa ofisini hainifai tena. Ninawahudumia lakini nani ananihudumia? Maisha haya ya kurejea nyumbani kutoka ofisini nikiwa nimechoka na bila pesa za kutosha kuilisha jamaa yangu yamenichosha.


Mshahara hautoshi, ushuru unapanda kila mwaka, bei ya unga imependa, gharama ya usafiri imepanda sana, licha ya kuwa nafanya kazi ngumu. Ninajiuzuru ili niweze kuyajali maslahi yangu na kujiendeleza kiuchumi. Ninataka kuwa mbunge wa eneo la Mashinani Kusini.


Funguo za ofisi nimemkabidhi msaidizi wako. Hii ndiyo siku yangu ya mwisho kazini. Naondoka bila kinyongo. Hata wale wenye fitina na ukorofi nimewasamehe. Ninajua nitarejea kuwaomba wachange pesa ili wanisaidie kupigania kitu hiki cha ubunge. Hata nawe mchango wako nitaufurahia. Sitowasahau nitakapokuwa Mbunge wa eneobunge la Mashinani Kusini.

Wako mtarajiwa

Mwizi wa Miwa.

 
 
 

Comentarios


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic

FOLLOW ME

  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • c-youtube

© 2023 by Samanta Jonse. Proudly created with Wix.com

bottom of page