top of page

Ngugi wa Thiong'o: Hadithi Mpya


Ngugi wa Thiong'o


Mwandishi mashuhuri kutoka Kenya, Profesa Ngugi wa Thiong'o, amechangia sana katika ukuzaji wa fasihi ya Kiafrika duniani. Lakini mchango wake mkubwa zaidi ni ule wa ukuzaji wa lugha za Kiafrika. Mchango wake wa hivi karibuni ni wa kihistoria: Hadithi yake mpya imetolewa kwa lugha 30 za Kiafrika. Na imetolewa kwa maandishi na pia kwa njia ya kimapokezi kama vile babu na nyanya zetu walitutambia hadithi. Hivi ni kusema kuwa hadithi mpya ya Ngugi imetafsiri na imerekodiwa katika lugha 30 kama vile Gikuyu, Kimarakwet, Kishona, Kiswahili, KiAmhara, Kihausa, Kindebele, Kinywaranda, na lugha zinginezo. Aidha hadithi imetafsiriwa kwa Kiingereza na Kifaransa ambazo ni lugha zinazozungumzwa sa barani Afrika. Fauka ya hayo, kuna tafsiri ya Sheng.



Hatuwezi kupuuza umuhimu wa hadithi ya Ngugi kutafsiriwa kwa lugha ya Sheng. Itakumbukwa kwamba katika miaka isiyokuwa mingi Sheng ilionekana kuwa lugha ya wahuni na vijana wasiokuwa na maadili wanaoishi jijini Nairobi. Wazazi na walimu waliwakanya watoto kusema lugha hii "chafu". Lakini tumeyaona mapinduzi ya kiisimu ambapo makumpuni yanatangaza bidhaa zao kwa kutumia Sheng, wanasiasa wanatumia Sheng kuwashawishi vijana wawapigie kura, hata Rais Barrack Obama wa Marekani aliwasalimia vijana kwa salamu za Sheng alipotembelea Kenya. Sasa bingwa wa mabingwa wa fasihi, Ngugi wa Thiong'o, amekubali hadithi yake itafsiriwe kwa Sheng.



Tangu alipoandika Decolonising the Mind na kuapa kuendelea kuandika kwa lugha ya mama, Gikuyu, badala ya lugha ya kikoloni, Kiingereza. Ngugi amefanya mchango mkubwa sana katika kuzipatia lugha za Kiafrika heshima inayostahili. Alichapisha jarida la kwanza la Gikuyu: Mutiiri. Baadaye akachapisha riwaya kubwa zaidi katika lugha za Kiafrika: Murogi wa Kagogo. Sasa hadithi hii ndiyo hadithi pekee ya Kiafrika yenye kutafsiriwa kwenye lugha nyingi hivyo.


Ngugi wa Thiong'o ni mtetezi mkubwa wa lugha na tamaduni za Kiafrika. Hata ingawa kamati ya kutunza Tuzo la Nobeli katika Fasihi halijamtunza bado, kwenye mioyo na bongo zetu, hakuna mwandishi bora zaidi ya Nguigi wa Thiong'o.


Vitabu vya Ngugi vimenikuza kimawazo na kimtazamo wa dunia tangu pale nilipokuwa mwanzafunzi wa fasihi na Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Baadaye nilipotunga tamthilia na hadithi zangu haikosi niliathiriwa na uandishi wa Ngugi. Nimefanikiwa kukutana naye mara tatu pamoja na kumwalika atembelee nyumbani kwangu kula chakula cha Kikenya.

 
 
 

Comentarios


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic

FOLLOW ME

  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • c-youtube

© 2023 by Samanta Jonse. Proudly created with Wix.com

bottom of page