ICC: Kiburi cha Bensouda na Ocampo
- Mungai Mutonya
- Apr 9, 2016
- 2 min read
Nilimsikiliza Fatou Bensouda alipotoa hotuba chuoni Washington alipofika kupewa tunzo na Idara ya Sheria. Wakati huo alikuwa naibu wa kiongozi mashaka ya mahakama ya ICC na kesi ya Kenya ilikuwa imetangazwa. Bensouda alifika na mumewe ambaye alikuwa Mkuu wa Sheria nchini Gambia. Alipofika alitoa hotuba kuu kuhusu sheria ya kimataifa na pia kukutana na makundi kadha chuoni wakiwemo wanafunzi wa Kiafrika. Alipata maswali mengi mazito na makali.

Kufuatia ziara yake na baada ya kutafakari mengi kuhusu kesi ya Kenya ambayo ilikwisha wiki hii baada ya mahakama ya ICC kutangaza kuwa Kaimu wa Rais wa Kenya, William Ruto, na mwanahabari, Joshua Sang, hawana kesi ya kujibu, nilikuwa na mawazo haya yafuatayo.
1) Nakubaliana na Waafrika wengi kuwa mahakama ya ICC imekuwa kifaa kingine cha kuendeleza ukoloni mamboleo barani Afrika. Mataifa ya kimagharibi yanatumia ICC kuendeleza maslahi yao ya kiuchumi na kisiasa barani Afrika. Nitarudia - maslahi ya kiuchumi na kisiasa. Waafrika Fatou Bensouda (kutoka) na Jaji Chile Ebou-Osuji (kutoka Nigeria) wamewekwa pale tu kutufumba macho. Sauti yao ni sauti ya wadhamini wa mahakama: nchi za kimagharibi. Hakuna la kuuliza wala kuficha. Mbona hatujawaona wale wanaondeleza unyama Iraq, Syria, Afghanistani, Palestine, na kwingineko mahakamani? Mbona wakoloni waliowauwa maelfu ya Waafrika enzi ya Mau Mau, Herero, Afrika Kusini, hawajahukumiwa.

2) Kiburi cha kikazi cha Moreno Ocampo na Fatou Bensouda kiliwaongoza badala ya ukweli wa kisheria. Moreno alikuwa anaiacha kazi ya Mkuu wa Mashtaka wa ICC na alitaka kuacha sifa kuwa alimshtaki rais mwafrika na makamu wake. Fatou naye alitaka kupata sifa kuwa alikuwa mkuu wa mashataka wa ICC aliyewafunga wakuu hao wa kiserikali kutoka Afrika. Umaarufu wa wanasheria hao wawili ungeongezeka sana na baadaye wangepewa nyadhifa kubwa zaidi. Aidha, Fatou alitoka nchi ndogo sana ya Gambia na alifikiri nchi kubwa za Kiafrika zina kiburi na zinazipuuza nchi ndogo. Kwenye hotuba yake alionekana kukerwa sana na ukweli Kenya ilidhubutu kumwalika rais wa Sudan, Omar Bashir, kuhudhuria sherehe nchini Kenya. Je, alifikiri viongozi wanaume wa Afrika walimdharau kwa vile ni mwanamke kutoka nchi ndogo na alitaka kudhihirisha uwezo wa cheo chake?
3) Moreno na Fatou walijitumbukiza kwenye siasa za ndani za Kenya wakitaka kujaribu kutumia mahakama kama kifaa cha kuwezesha kuchaguliwa kwa viongozi wanaopendelewa na nchi za Magharibi. Wakishirikiana na vibaraka Wakenya wenye kudhaminiwa na mataifa ya Magharibi na wenye kijivisha mavuzi ya Civil Society (au Evil Society kama ijulikanavyo Kenya) ICC ingetumika kuhakikisha kuwa Uhuru Kenyatta na William Ruto hawangesimama uchaguzi. Wakisimama, kesi ya ICC ingewaharibia sifa na wangeshindwa na kuwezesha kiongozi aliyependelewa kushinda. Mpango ungalifaulu Kenya, ungalitumika kwingineko. Lakini mpango ulitumbikia nyongo kesi ya ICC ilipowapa wakenya fursa ya kupinga njama za wana-ukolonimamboleo hao. Uhuru na Ruto wakapata ushindi.
4) Kinyume na walivyotarajia wapanga mikakati wakoloni hao, kesi ya ICC dhidi ya rais Uhuru Kenyatta na makamu wake Ruto imechangia kuliunganisha zaidi bara la Afrika.
Waswahili husema, mchimba kaburi huingia mwenyewe.
Blogu safi sana, imekua kitambo tangu nisome blogu la Kiswahili.