Prince Aaga Dunia
- Mungai Mutonya
- Apr 21, 2016
- 1 min read

Mwanamuziki mashuhuri ajulikanaye kwa jina maarafu 'Prince' ameaga dunia. Ni huzuni kubwa kwetu mashabiki wa muziki wake. Alipatikana amekufa nyumbani kwake katika jimbo la Minnesota. Alikuwa na umri wa miaka 57. Ni siku chache tu zilizopita aliwatumbuiza maelfu ya mashabiki wake mjini Atlanta. Hata juzi aliwandalia marafiki zake karamu nyumbani kwake. Je, alijua sabbat ya kuandaa karamu hiyo?
Alifikiriwa kuwa mwenye afya nzuri, ingawa alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kuwatumbuiza watu Atlanta, ndege yake ilitua ghafla katika jimbo la Indiana kusudi apate matibabu ya dharura. Alisemekana alikuwa amepoteza fahamu na kuwa aliugua homa.
Prince alikuwa mwanamuziki tuliyemuenzi sana katika ujana wangu. Tulivutiwa sana na muziki wake na ule wa Michael Jackson. Mimi niliwaona kuwa kama ndugu kwa vile walivyofanana. Sura zao. Mavazi yao. Ustadi wao wa kucheza dansi. Hata muziki ulifanana kwa kiasi.
Nilimpenda Prince zaidi kwa vile msichana fulani rafiki yangu aliniimbia wimbo wake 'When Doves Cry.' Ulikuwa ni wakati mgumu maishani yangu ya ujana na wimbo huo uliniletea raha ya kipekee moyoni. Mpaka sasa wimbo huo ni kati ya nyimbo zenye kumbukumbu maalum maishani mwangu.
Ninamuaga Prince kwa kusema kuwa mvua ya zambarau (Purple Rain) inanyesha na njiwa wanalia (Doves Cry). Buriani msanii wenye taaluma ya kipekee, Prince.
Comentários