top of page

Kiswahili na Kikalenjin katika Olimpiki

Olimpiki 2016 inabisha hodi. David Rudisha atairudisha dhahabu nyumbani. Kemboi atacheza rumba ya ushindi. Hussein Bolt atatimuka kama radi. Wakenya na Waethiopia wataonyesha ufalme wao kwenye mbio za masafa marefu. Tutajivunia ushindi wao. Tutashangilia mashindano kwenye runinga zetu. Halafu tutacheka watakapokuwa wanahojiwa kwa Kiingereza. Tutatamani waseme Kiswahili, Kikalenjin, Kiamhara, au Kinyarwanda halafu matamshi yao yatafsiriwe kwa Kiingereza. Wakisema lugha zao hawatachekwa wala vibonzo havitawakejeli.

Kwa nini ninatoa kauli hiyo? Kumbuka yaliyotendeka wiki iliyopita nchini Poland. Jean Marie Myasiro, kijana Mnyarwanda mwenye umri wa miaka 19, aliivunjika rekodi ya kitaifa ya Rwanda kwenye mbio za mita 10,000. Rekodi ya awali iliwekwa mwaka 2004 na Mnyarwanda mwenzake, Valence Bihavagamuye. Jean Marie alivuma sana kwenye mitandao ya kijamii wiki jana. Lakini hakupata umaarufu kwa ushindi huu. Ushindi alioupata kwenye mashindano ya dunia ya IAAF ya vijana wenye umri chini ya miaka 20. Mashindano yaliyofanyika mjini Bydgoszcz, nchini Poland. La hasha, Jean Marie hakupata umaarufu na kushangiliwa na kwenye mitandao kwa uhodari huu. Lakini alipata umaarufu huo eti kwa kusema Kiingereza kibaya.

Wengi wamekuwa wakimcheka na wengine kumkemea kwa kusema Kiingereza vibaya. Vidio ya mahojiano yake baada ya kumaliza mbio iliisambazwa kwa wingi katika WhatsApp, Facebook, Twitter, na kadhalika.

Watu hawakujali kuwa kijana huyu aliwashinda wengi ili kufuzu kushiriki mashindano ya dunia. Hawakujali aliivunja rekodi ya kitaifa ya Rwanda. Hawakujali iwapo anasema lugha zingine kama vile Kinyarwanda, Kiswahili, Kirundi, Kifaransa au lugha nyinginezo. Walijali tu kuwa alisema Kiingereza kibaya.

Imekuwa kawaida kuwacheka wanariadha wetu wanapohojiwa na wanahabari baada ya ushindi wao. Swali ambalo mimi hujiuliza ni kwa nini huwajielezi kwa lugha zao? Messi husema kihispania kwenye mahojiano yote kila mara. Na ndiye mwanasoka bora zaidi duniani. Wachina, Warusi, Waarabu, Wajapani na wengineo wanasema lugha zao na wanahabari wanatafuta wakalimani kutafsiri. Waafrika pekee ndio wanang'ang'ana kusema kiingereza na Kifaransa.

Olimpiki yaja. Wanariadha wetu Waafrika wasema Kikalenjin, Kimaasai, Ekegusii, Kinyarwanda, Luganda, Kiamhara, Kizulu na lugha zingine za Kiafrika wanapohojiwa. Hakuna mtu atawacheka. Hawatajiaibisha. Watahifadhi hadhi na heshima yao. Tujivunie lugha. zetu.



 
 
 

Comments


Featured Posts
Recent Posts
Search By Tags
Follow Us
  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • Google Classic

FOLLOW ME

  • Facebook Classic
  • Twitter Classic
  • c-youtube

© 2023 by Samanta Jonse. Proudly created with Wix.com

bottom of page